(119) Kisha hakika Mola wako Mlezi kwa walio tenda uovu kwa ujinga, kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema; bila ya shaka Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.
(120) Hakika Ibrahim alikuwa mfano mwema, mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
(121) Mwenye kuzishukuru neema zake, Mwenyezi Mungu. Yeye kamteuwa, na akamwongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka.
(122) Na tukampa wema duniani, na hakika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
(123) Kisha tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibrahim, mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
(124) Hakika siku ya Sabato (Jumaamosi) waliwekewa wale walio khitalifiana kwa ajili yake. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitalifiana.
(125) Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.
(126) Na mkilipiza basi lipizeni sawa na vile mlivyo adhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanao subiri.
(127) Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe ila kwa sababu ya Mwenyezi Mungu tu. Wala usiwahuzunikie; wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazo zifanya.
(128) Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kumcha, na watendao mema.