(100) Na wale walio tangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na walio wafuata kwa wema, Mwenyezi Mungu ameridhika nao, na wao wameridhika naye; na amewaandalia Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
(101) Na katika mabedui walio jirani zenu wamo wanaafiki; na katika wenyeji wa Madina pia wapo walio bobea katika unaafiki. Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.
(102) Na wengine walikiri dhambi zao, wakachanganya vitendo vyema na vingine viovu. Asaa Mwenyezi Mungu akapokea toba zao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
(103) Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
(104) Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anapokea toba ya waja wake, na anazikubali sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba na Mwenye kurehemu?
(105) Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini wataviona vitendo vyenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye kujua siri na dhaahiri; naye atakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.
(106) Na wapo wengine wanangojea amri ya Mwenyezi Mungu - ama atawaadhibu au atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.