(69) Ni kama wale walio kuwa kabla yenu. Walikuwa wana nguvu na mali na watoto zaidi kuliko nyinyi. Basi walistarehea fungu lao, na nyinyi mnastarehea fungu lenu, kama walivyo starehe kwa fungu lao wale walio kuwa kabla yenu. Na nyinyi mkazama katika maovu kama wao walivyo zama. Hao ndio ambao vitendo vyao vimeharibika katika dunia na Akhera; na hao ndio walio khasiri.
(70) Je, hazikuwafikia khabari za walio kuwa kabla yao - kaumu ya Nuhu, na A'ad, na Thamud, na kaumu ya Ibrahim, na watu wa Madyana, na miji iliyo pinduliwa chini juu? Mitume wao waliwafikia kwa hoja zilizo wazi. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, walakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
(71) Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zaka, na humt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(72) Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini wanaume na Waumini wanawake Bustani zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na makaazi mema katika Bustani za kudumu, na Radhi za Mwenyezi Mungu ndio kubwa kuliko yote. Huko ndiko kufuzu kukubwa.