(123) Enyi mlio amini! Piganeni na wale makafiri walio karibu yenu, na wakute ugumu kwenu. Na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wacha- Mngu.
(124) Na inapo teremshwa Sura wapo miongoni mwao wasemao: Ni nani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia Imani? Ama wale walio amini inawazidishia Imani, nao wanafurahi.
(125) Ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi inawazidishia uovu juu ya uovu wao; na wanakufa hali ni makafiri.
(126) Je! Hawaoni ya kwamba wanatiwa mtihanini kila mwaka mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu, wala hawakumbuki.
(127) Na ikiteremka Sura hutazamana wao kwa wao, (kama kwamba wanasema:) Je! Yuko mtu anakuoneni? Kisha hugeukilia mbali. Mwenyezi amezigeuza nyoyo zao kwa kuwa hao ni watu wasio fahamu.
(128) Hakika amekwisha kujieni Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yanayo kutaabisheni; anakuhangaikieni sana. Kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.
(129) Basi wakigeuka, wewe sema: Mwenyezi Mungu ananitosheleza. Hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mimi namtegemea Yeye, na Yeye ndiye Mola Mlezi wa Kiti Kikuu cha Enzi.