(62) Wanakuapieni Mwenyezi Mungu ili kukuridhisheni nyinyi, hali ya kuwa wanao stahiki zaidi kuridhishwa ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lau kama wao ni Waumini.
(63) Je, hawajui ya kwamba anaye shindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata Moto wa Jahannamu adumu humo? Hiyo ndiyo hizaya kubwa.
(64) Wanaafiki wanaogopa isije teremshwa Sura itakayo watajia yaliyomo katika nyoyo zao. Sema: Fanyeni mzaha! Hakika Mwenyezi Mungu atayatoa nje hayo mnayo yaogopa.
(65) Na ukiwauliza, wanasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na kucheza tu. Sema: Mlikuwa mkimfanyia maskhara Mwenyezi Mungu na Ishara zake na Mtume wake?
(66) Msitoe udhuru; mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu! Tukilisamehe kundi moja kati yenu, tutaliadhibu kundi jingine kwa kuwa wao ni wakosefu.
(67) Wanaume wanaafiki na wanawake wanaafiki, wote ni hali moja. Huamrisha maovu na huyakataza mema, na huifumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia amewasahau. Hakika wanaafiki ndio wapotofu.
(68) Mwenyezi Mungu amewaahidi wanaafiki wanaume na wanaafiki wanawake na makafiri Moto wa Jahannamu kudumu humo. Hayo yanawatosha, na Mwenyezi Mungu amewalaani; nao wana adhabu milele.