(112) (Kwa) wanao tubia, wanao abudu, wanao himidi, wanao kimbilia kheri, wanao rukuu, wanao sujudu, wanao amrisha mema na wanao kataza maovu, na wanao linda mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na wabashirie Waumini.
(113) Haimpasii Nabii na wale walio amini kuwatakia msamaha washirikina, ijapo kuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa hao ni watu wa Motoni.
(114) Wala haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila kwa sababu wa ahadi aliyo fanya naye. Lakini ilipo mbainikia kwamba yeye ni adui ya Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye. Hakika Ibrahim alikuwa mwingi wa kuomba, mnyenyekevu, mvumilivu.
(115) Na haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwahisabu watu kuwa wamepotea baada ya kwisha waongoza mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
(116) Hakika Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu na ardhi; huhuisha na hufisha. Nanyi hamna Mlinzi wala Msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
(117) Mwenyezi Mungu amekwisha pokea toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari walio mfuata katika saa ya dhiki, pale baada ya kukaribia nyoyo za baadhi yao kugeuka. Basi akapokea toba yao, kwani hakika Yeye kwao wao ni Mpole na ni Mwenye kuwarehemu.