(80) Waombee msamaha au usiwaombee. Hata ukiwaombea msamaha mara sabiini, Mwenyezi Mungu hatawasamehe. Hayo ni kwa sababu ya kuwa wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotofu.
(81) Walifurahi walio achwa nyuma kwa kule kubakia kwao nyuma na kumuacha Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na walichukia kupigana Jihadi kwa mali zao na nafsi zao, na wakasema: Msitoke nje katika joto! Sema: Moto wa Jahannamu una joto zaidi, laiti wangeli fahamu!
(82) Basi nawacheke kidogo; watalia sana. Hayo ni malipo ya yale waliyo kuwa wakiyachuma.
(83) Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kikundi kimoja miongoni mwao - na wakakutaka idhini ya kutoka - sema: Nyinyi hamtatoka pamoja nami kabisa, wala hamtapigana na adui pamoja nami. Nyinyi mliridhia kukaa nyuma mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na hao watakao bakia nyuma.
(84) Wala usimsalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala usisimame kaburini kwake. Hakika hao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakafa na hali ni wapotofu.
(85) Wala zisikushitue mali zao na watoto wao. Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwa hayo katika dunia; na zitoke roho zao na hali wao ni makafiri.
(86) Na inapo teremshwa Sura isemayo: Muaminini Mwenyezi Mungu na piganeni Jihadi pamoja na Mtume wake, wale wenye nguvu miongoni mwao hukutaka ruhusa na husema: Tuache tuwe pamoja na wanao kaa nyuma!