(84) Na unijaalie nitajwe kwa wema na watu watakao kuja baadaye.
(85) Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.
(86) Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.
(87) Wala usinihizi Siku watapo fufuliwa.
(88) Siku ambayo kwamba mali hayato faa kitu wala wana.
(89) Isipo kuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.
(90) Na Pepo itasogezwa kwa wachamngu.
(91) Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.
(92) Na wataambiwa: Wako wapi mlio kuwa mkiwaabudu
(93) Badala ya Mwenyezi Mungu? Je! Wanakusaidieni, au wanajisaidia wenyewe?
(94) Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu,
(95) Na majeshi ya Ibilisi yote.
(96) Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:
(97) Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhaahiri,
(98) Tulipo kufanyeni ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(99) Na hawakutupoteza ila wale wakosefu.
(100) Basi hatuna waombezi.
(101) Wala rafiki wa dhati.
(102) Laiti tungeli pata kurejea tena tungeli kuwa katika Waumini.
(103) Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
(104) Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kurehemu.
(105) Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.
(106) Alipo waambia ndugu yao, Nuhu: Je! Hamchimngu?
(107) Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
(108) Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.
(109) Na sikutakini juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(110) Basi Mcheni Mwenyezi Mungu, na nit'iini mimi.
(111) Wakasema: Je! Tukuamini wewe, hali wanao kufuata ni watu wa chini?