(141) Na pia ili Mwenyezi Mungu awasafishe walio amini na awafutilie mbali makafiri.
(142) Je! Mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawapambanua wale miongoni mwenu walio pigana Jihadi, na hajawapambanua walio subiri?
(143) Na nyinyi mlikuwa mkitamani mauti kabla hamjakutana nayo. Basi sasa mmekwisha yaona na huku mnayatazama.
(144) Na Muhammad hakuwa ila ni Mtume tu. Wamekwisha pita kabla yake Mitume. Je, akifa au akauwawa ndiyo mtageuka mrudi nyuma? Na atakaye geuka akarudi nyuma huyo hatamdhuru kitu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu atawalipa wanao mshukuru.
(145) Na haiwezi nafsi kuwa ife ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu kama ilivyo andikwa ajali yake. Na mwenye kutaka malipo ya duniani tutampa; na mwenye kutaka malipo ya Akhera tutampa. Na tutawalipa wenye kushukuru.
(146) Na Manabii wangapi walipigana na pamoja nao Waumini wengi wenye ikhlasi! Hawakufanya woga kwa yaliyo wasibu katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawakudhoofika wala hawakuwa wanyonge. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wanao subiri.
(147) Wala kauli yao haikuwa ila ni kusema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie madhambi yetu na kupita kwetu kiasi katika mambo yetu, na isimamishe imara miguu yetu na utunusuru tuwashinde kaumu ya makafiri.
(148) Basi Mwenyezi Mungu akawapa malipo ya duniani na bora ya malipo ya Akhera. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wafanyao mema.