(122) Makundi mawili miongoni mwenu yakaingiwa na woga kuwa watashindwa - na hali Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wao; na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu.
(123) Na Mwenyezi Mungu alikwisha kunusuruni katika Badri nanyi mlikuwa wanyonge. Basi mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kushukuru.
(124) Ulipo waambia Waumini: Je, haitakutosheni ikiwa Mola wenu atakusaidieni kwa Malaika elfu tatu walio teremshwa?
(125) Kwani! Ikiwa mtavumilia na mkamchamngu na hata maadui wakikutokeeni kwa ghafla, basi hapo Mola wenu Mlezi atakusaidieni kwa Malaika elfu tano wanao shambulia kwa nguvu.
(126) Na Mwenyezi Mungu hakufanya haya ila kuwa ni bishara kwenu, na ili nyoyo zenu zipate kutua. Na msaada hautoki isipo kuwa kwa Mwenyezi Mungu, Aliye tukuka, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
(127) Haya ni kwa ajili awakate sehemu katika walio kufuru, au awahizi wapate kurejea nyuma nao wamepwelewa.
(128) Wewe huna lako jambo katika haya - ama atawahurumia au atawaadhibu, kwani wao ni madhaalimu.
(129) Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Yeye humsamehe na humuadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Msamehevu Mwenye kurehemu.
(130) Enyi mlio amini! Msile riba mkizidisha juu kwa juu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
(131) Na uogopeni Moto ambao umeandaliwa kwa ajili ya makafiri.
(132) Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume ili mpate kurehemewa.