(116) Hakika wale walio kufuru hazitawafaa kitu mali zao wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio watu wa Motoni - humo watadumu.
(117) Mfano wa vile wanavyo vitoa katika uhai wao wa duniani ni kama upepo ambao ndani yake ipo baridi ya barafu, ukalisibu shamba la watu walio dhulumu nafsi zao, ukaliteketeza. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, bali wao wenyewe wanadhulumu nafsi zao.
(118) Enyi mlio amini! Msiwafanye wasiri wenu watu wasio kuwa katika nyinyi. Hawataacha kukufanyieni ubaya. Wanayapenda yanayo kudhuruni. Imekwisha fichuka chuki yao katika midomo yao. Na yanayo ficha vifua vyao ni makubwa zaidi. Tumekwisha kubainishieni Ishara ikiwa nyinyi mtayatia akilini.
(119) Hivyo basi nyinyi ndio mnawapenda watu hao, wala wao hawakupendeni. Nanyi mnaviamini Vitabu vyote. Na wanapo kutana nanyi husema: Tumeamini. Na wanapo kuwa peke yao wanakuumieni vidole kwa chuki. Sema: Kufeni kwa chuki yenu! Hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliomo vifuani.
(120) Ikikupateni kheri huwaudhi. Na ikikupateni shari wanafurahia. Na nyinyi mkisubiri na mkajizuilia, hila zao hazitakudhuruni kitu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyazunguka yote wayatendayo.
(121) Na pale ulipo toka asubuhi, ukaacha ahali zako uwapange Waumini kwenye vituo kwa ajili ya vita - na Mwenyezi Mungu anasikia na anajua.