آل عمران Aal-Imran
(1) Alif Laam Miim.
(2) Mwenyezi Mungu, hakuna mungu ila Yeye Aliye Hai, Msimamizi wa yote milele.
(3) Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinacho sadikisha yaliyo kuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili
(4) Kabla yake, ziwe uwongofu kwa watu. Na akateremsha Furqani (Upambanuo). Hakika walio zikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu watakuwa na adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye kulipa.
(5) Hakika Mwenyezi Mungu hakifichiki chochote kwake, duniani wala mbinguni.
(6) Yeye ndiye anaye kuundeni ndani ya matumbo ya wazazi kwa namna apendayo. Hapana mungu ila Yeye, Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
(7) Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam, zenye maana wazi. Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano. Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipo kuwa wenye akili.
(8) (Na hao husema): Mola wetu Mlezi! Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kwisha tuongoa, na utupe rehema itokayo kwako. Hakika Wewe ndiye Mpaji.
(9) Mola wetu Mlezi! Wewe ndiye Mkusanyaji wa watu kwa Siku isiyo na shaka ndani yake. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.