(158) Na mkifa au mkiuliwa ni kwa Mwenyezi Mungu ndio mtakusanywa.
(159) Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo. Na ukisha kata shauri basi mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wanao mtegemea.
(160) Akikunusuruni Mwenyezi Mungu hapana wa kukushindeni, na akikutupeni ni nani, basi, baada yake Yeye ataye kunusuruni? Na Waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu tu.
(161) Na haiwezekani kwa Nabii yeyote kufanya khiyana. Na atakaye fanya khiyana, atayaleta Siku ya Kiyama aliyo yafanyia khiyana, kisha kila mtu atalipwa kwa aliyo yachuma, kwa ukamilifu; wala hawatadhulumiwa.
(162) Je! Aliye yafuata ya kumridhisha Mwenyezi Mungi ni kama yule aliye stahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, na makaazi yake yakawa Jahannamu? Napo ni mahala pabaya pa kurejea.
(163) Hao wana vyeo mbali mbali kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona yote wayatendayo.
(164) Hakika Mwenyezi Mungu amewafanyia wema mkubwa Waumini vile alivyo waletea Mtume aliye miongoni mwao wenyewe, anaye wasomea Aya zake, na anawatakasa, na anawafunza Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya hapo walikuwa katika upotovu ulio wazi.
(165) Nyinyi - ulipo kusibuni msiba ambao nyinyi mmekwisha watia mara mbili mfano wa huo - mnasema: Umetoka wapi huu? Sema: Huo umetoka kwenu wenyewe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.