(187) Na pale Mwenyezi Mungu alipo fungamana na walio pewa Kitabu kuwa: Lazima mtawabainishia watu, wala hamtokificha, walikitupa nyuma ya migongo yao, na wakanunua kwacho thamani duni. Basi ni kiovu hicho walicho nunua.
(188) Usiwadhanie kabisa wale wanao furahia waliyo yafanya, na wakapenda kusifiwa kwa wasiyo yatenda, usiwadhanie kuwa watasalimika na adhabu. Yao wao ni adhabu chungu.
(189) Na Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
(190) Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko Ishara kwa wenye akili,
(191) Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto.
(192) Mola wetu Mlezi! Hakika unaye mtia Motoni umemhizi; na walio dhulumu hawana wasaidizi.
(193) Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tumemsikia mwenye kuita akiitia Imani kwamba: Muaminini Mola wenu Mlezi; nasi tukaamini. Basi tusamehe madhambi yetu, na utufutie makosa yetu, na utufishe pamoja na watu wema.
(194) Mola wetu Mlezi! Na utupe uliyo tuahidi kwa Mitume wako, wala usituhizi Siku ya Kiyama. Hakika Wewe huvunji miadi.