(10) Kwa hakika wale walio kufuru hazitowafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu mali zao, wala watoto wao; nao hao ndio kuni za Motoni-
(11) - Kama yaliyo wapata watu wa Firauni na wale walio kuwa kabla yao. Walikanusha Ishara zetu, basi Mwenyezi Mungu aliwashika kwa madhambi yao; na Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
(12) Waambie walio kufuru: Karibuni mtashindwa na mtakusanywa, mtiwe kwenye Jahannam; nako huko ni makao mabaya kabisa.
(13) Hakika ilikuwa ni Ishara kwenu katika yale majeshi mawili yalipo pambana. Jeshi moja likipigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jingine kafiri likiwaona zaidi kuliko wao mara mbili, kwa kuona kwa macho. Na Mwenyezi Mungu humuunga mkono amtakaye kwa nusura yake. Hakika katika hayo yapo mazingatio kwa wenye macho.
(14) Watu wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni starehe ya maisha ya duniani; na kwa Mwenyezi Mungu ndio kwenye marejeo mema.
(15) Sema: Nikwambieni yaliyo bora kuliko hayo? Kwa wachamngu ziko Bustani kwa Mola wao zipitazo mito kati yake. Watadumu humo, na wake walio takaswa, na wanazo radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake,