(171) Na pale tulipo unyanyua mlima juu yao ukawa kama kwamba ni kiwingu kilicho wafunika, na wakadhani kuwa utawaangukia, (tukawaambia): Kamateni kwa nguvu tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kumcha Mungu.
(172) Na pale Mola wako Mlezi alipo waleta katika wanaadamu kutoka migongoni mwao kizazi chao, na akawashuhudisha juu ya nafsi zao, akawaambia: Je, Mimi si Mola Mlezi wenu? Wakasema: Kwani! Tumeshuhudia. Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo.
(173) Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu?
(174) Ndio kama hivyo tunavyo zipambanua Ishara, kwa kutaraji kuwa watarejea.
(175) Na wasomee khabari za yule ambaye tulimpa Ishara zetu, naye akajivua nazo. Na Shet'ani akamuandama, akawa miongoni walio potea.
(176) Na tungelitaka tungeli mtukuza kwa hizo Ishara, lakini yeye aliushikilia ulimwengu na akafuata pumbao lake. Basi mfano wake ni mfano wa mbwa. Ukimhujumu hupumua na kutoa ulimi na ukimwacha pia hupumua na kutoa ulimi. Huo ni mfano wa kaumu wanao zikanusha Ishara zetu. Basi simulia hadithi, huenda wakatafakari.
(177) Huu ni mfano muovu kabisa wa watu wanao kanusha Ishara zetu na wakajidhulumu nafsi zao.
(178) Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemhidi basi huyo amehidika; na alio waacha kupotea basi hao ndio walio khasirika.