(179) Na tumeiumbia Jahannamu majini wengi na watu. Wana nyoyo, lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama nyama howa, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walio ghafilika.
(180) Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwa hayo. Na waacheni wale wanao haribu utakatifu wa majina yake. Hao watakuja lipwa waliyo kuwa wakiyatenda.
(181) Na katika tulio waumba wako watu wanao ongoza kwa Haki, na kwayo wanafanya uadilifu.
(182) Na wale walio kadhibisha Ishara zetu, tutawapururia pole pole kwa namna ambayo wenyewe hawaijui.
(183) Nami nitawapa muda. Hakika mpango wangu ni madhubuti.
(184) Je, hawafikiri? Huyu mwenzao hana wazimu. Hakuwa yeye ila ni mwonyaji aliye dhaahiri.
(185) Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi, na vitu alivyo viumba Mwenyezi Mungu, na pengine ajali yao imekwisha karibia? Basi maneno gani baada ya haya watayaamini?
(186) Aliye mwacha Mwenyezi Mungu kupotea hana wa kumwongoa. Atawaacha hao wakitangatanga katika upotofu wao.
(187) Wanakuuliza hiyo Saa (ya mwisho) itakuwa lini? Sema: Kuijua kwake kuko kwa Mola Mlezi wangu. Haidhihirishi hiyo kwa wakati wake ila Yeye. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haikujiini ila kwa ghafla tu. Wanakuuliza kama kwamba wewe una pupa ya kuijua. Sema: Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu. Lakini aghlabu ya watu hawajui.