(188) Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu ninge jizidishia mema mengi, wala ovu lisinge nigusa. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mbashiri kwa watu wanao amini.
(189) Yeye ndiye aliye kuumbeni katika nafsi moja; na katika hiyo hiyo akamfanya mwenzi wake, ili akae naye kwa utulivu. Na anapo muingilia hubeba mzigo mwepesi, akitembea nao. Anapo kuwa mja mzito, wote wawili humwomba Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wao: Kama ukitupa mwana mwema tutakuwa katika wanao shukuru.
(190) Basi anapo wapa mwana mwema, wanamfanyia washirikina Mwenyezi Mungu katika kile kile alicho wapa. Mwenyezi Mungu ametukuka na huko kushirikisha kwao.
(191) Ati wanawafanya viumbe kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu, nao hawaumbi, bali wao ndio wanaumbwa?
(192) Wala hawana uwezo wa kuwanusuru wala wenyewe hawajinusuru.
(193) Na mkiwaita kwenye uwongofu, hawakufuateni. Ni mamoja kwenu ikiwa mtawaita au mkinyamaza.
(194) Hakika hao mnao waomba asiye kuwa Mwenyezi Mungu ni waja mfano wenu nyinyi. Hebu waombeni, nao wakuitikieni, kama mnasema kweli.
(195) Je, wao wanayo miguu ya kwendea? Au wanayo mikono ya kutetea? Au wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikizia? Sema: Iiteni hio miungu yenu ya ushirikina. Kisha nifanyieni mimi vitimbi, wala msinipe muhula.