(52) Na hakika tumewaletea Kitabu tulicho kipambanua kwa ilimu, uwongofu na rehema kwa watu wenye kuamini.
(53) Je, lipo wanalo lingojea isipo kuwa matokeo yake? Siku yatapo fika matokeo yake watasema wale walio kisahau: Kweli Mitume wa Mola Mlezi wetu walileta Haki! Je, tunao waombezi ili watuombee? Au turudishwe ili tufanye yasiyo kuwa yale tuliyo kuwa tukiyafanya? Bila ya shaka wamejikhasiri nafsi zao, na yamewapotea waliyo kuwa wakiyazua.
(54) Hakika Mola Mlezi wenu ni Mwenyezi Mungu aliye ziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazo tumika kwa amri yake. Fahamuni! Kuumba na amri ni zake. Ametukuka kabisa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
(55) Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa siri. Hakika Yeye hawapendi warukao mipaka.
(56) Wala msifanye uharibifu katika nchi baada ya kuwa imekwisha tengenezwa. Na muombeni kwa kuogopa na kwa kutumai. Hakika rehema ya Mwenyzi Mungu iko karibu na wanao fanya mema.
(57) Na Yeye ndiye anaye peleka pepo (za kuvuma) kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata hizo pepo zinapo beba mawingu mazito tunayachunga mpaka kwenye nchi iliyo kufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, ndio kama hivyo tukatolesha kila aina ya matunda. Basi hali kadhaalika tunavyo wafufua wafu, ili mpate kukumbuka.