(31) Enyi wanaadamu! Chukueni pambo lenu kwenye kila pahala wakati wa ibada, na kuleni, na kunyweni na wala msifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanao fanya israfu.
(32) Sema: Ni nani aliye harimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilo watolea waja wake, na vilivyo vizuri katika riziki. Sema hivyo ni kwa walio amini katika uhai wa duniani, na Siku ya Kiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivi tunazieleza Ishara kwa watu wanao jua.
(33) Sema: Mola Mlezi wangu ameharimisha mambo machafu ya dhaahiri na ya siri, na dhambi, na uasi bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na asicho kiletea uthibitisho, na kumzulia Mwenyezi Mungu msiyo yajua.
(34) Na kila umma una muda wake. Utakapo fika muda wao basi hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia.
(35) Enyi wanaadamu! Watakapo kufikieni Mitume miongoni mwenu wakakuelezeni Ishara zangu, basi watakao mchamngu na wakatengenea haitakuwa khofu kwao, wala hawatahuzunika.
(36) Na wale watakao kanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hao ni watu wa Motoni; humo watadumu.
(37) Basi ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, au anaye zikanusha Ishara zake? Hao itawafikia sehemu yao waliyo andikiwa, mpaka watakapo wafikia wajumbe wetu kuwafisha, watawaambia: Wako wapi mlio kuwa mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea! Na watajishuhudia wenyewe kwamba walikuwa makafiri.