(38) Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni Motoni pamoja na umma zilizo pita kabla yenu za majini na watu. Kila utakapo ingia umma utawalaani wenzake. Mpaka watakapo kusanyika wote humo, wa mwisho wao watawasema wa mwanzo wao: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio walio tupoteza; basi wape adhabu ya Motoni marudufu. Atasema: Itakuwa kwenu nyote marudufu, lakini nyinyi hamjui tu.
(39) Na wa mwanzo wao watawaambia wa mwisho wao: Basi nyinyi pia hamkuwa na ubora kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyachuma.
(40) Hakika wale wanao zikanusha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Peponi mpaka apite ngamia katika tundu ya sindano. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wakosefu.
(41) Jahannamu itakuwa kitanda chao na juu yao nguo za moto za kujifunika. Na hivi ndivyo tunavyo walipa madhaalimu.
(42) Na wale wanao amini na wakatenda mema - hatumkalifishi mtu yoyote ila kwa kiasi cha uwezo wake - hao ndio watu wa Peponi. Wao watadumu humo.
(43) Na tutaondoa chuki vifuani mwao, na mbele yao iwe inapita mito. Na watasema: Alhamdulillah! Kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliye tuhidi kufikia haya. Wala hatukuwa wenye kuhidika wenyewe ingeli kuwa Mwenyezi Mungu hakutuhidi. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walileta Haki. Na watanadiwa kwamba: Hiyo ndiyo Pepo mliyo rithishwa kwa sababu ya mliyo kuwa mkiyafanya.