(9) Na kama tungeli mfanya Malaika bila ya shaka tungeli mfanya kama binaadamu, na tungeli watilia matatizo yale wanayo yatatiza wao.
(10) Na hakika Mitume walio kabla yako walifanyiwa kejeli, lakini walio wafanyia kejeli wakaja kuzungukwa na yale yale waliyo kuwa wao wanayafanyia kejeli.
(11) Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha.
(12) Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. Hakika atakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo kuwa na shaka. Walio jikhasiri wenyewe hawaamini.
(13) Na ni vyake vilio tulia usiku na mchana. Naye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
(14) Sema: Je, nimchukue rafiki mlinzi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba mbingu na ardhi, naye ndiye anaye lisha wala halishwi? Sema: Mimi nimeamrishwa niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa usiwe miongoni wa washirikina.
(15) Sema: Mimi naogopa adhabu ya Siku kubwa hiyo ikiwa nitamuasi Mola wangu Mlezi.
(16) Siku hiyo yule atakaye epushwa nayo adhabu hiyo atakuwa Mwenyezi Mungu amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kulio wazi.
(17) Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusisha madhara, basi hapana wa kukuondolea hayo ila Yeye. Na ikiwa akikugusisha kheri, basi Yeye ndiye Mwenye uweza wa kila kitu.
(18) Naye ndiye Mwenye nguvu juu ya waja wake, na ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari zote.