(147) Wakikukanusha basi wewe sema: Mola Mlezi wenu ni Mwenye rehema iliyo enea. Wala haizuiliki adhabu yake kwa watu wakhalifu.
(148) Watasema walio shirikisha: Lau kuwa Mwenyezi Mungu ange taka tusingeli shiriki sisi, wala baba zetu; wala tusingeli harimisha kitu chochote. Vivi hivi walikanusha walio kuwa kabla yao mpaka walipo onja adhabu yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo ilimu mtutolee? Nyinyi hamfuati ila dhana. Wala hamsemi ila uwongo tu.
(149) Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye hoja ya kukata. Na kama angeli penda angeli kuhidini nyote.
(150) Sema: Leteni mashahidi wenu watao shuhudia kuwa Mwenyezi Mungu ameharimisha hawa. Basi wakishuhudia, wewe usishuhudie pamoja nao. Wala usifuate matamanio ya walio zikanusha Ishara zetu, wala hawaiamini Akhera, na ambao wanamlinganisha Mola Mlezi wao na wengine.
(151) Sema: Njooni nikusomeeni aliyo kuharimishieni Mola wenu Mlezi. Nayo ni kuwa, msimshirikishe Yeye na chochote. Na wazazi wenu wafanyieni wema. Wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunakuruzukuni nyinyi na wao. Wala msikaribie mambo machafu, yanayo onekana, na yanayo fichikana. Wala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu ameharimisha kuiuwa, ila ikiwa kwa haki. Hayo amekuusieni ili myatie akilini.