(60) Naye ndiye anaye kufisheni usiku, na anakijua mlicho fanya mchana. Kisha Yeye hukufufueni humo mchana ili muda ulio wekwa utimizwe. Kisha kwake Yeye ndiyo marejeo yenu, na tena akwambieni mliyo kuwa mkiyafanya.
(61) Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya waja wake. Na hukupelekeeni waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha, nao hawafanyi taksiri.
(62) Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki. Hakika, hukumu ni yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanao hisabu.
(63) Sema: Ni nani anaye kuokoeni katika giza la nchi kavu na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa siri, mkisema: Kama akituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanao shukuru.
(64) Sema: Mwenyezi Mungu hukuokoeni kutoka hayo, na kutoka kila mashaka, na kisha nyinyi mnamshirikisha!
(65) Sema: Yeye ndiye Muweza wa kukuleteeni adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu, au kukuleteeni fujo la mfarakano, na kuwaonjesha baadhi yenu jeuri ya wenzao. Tazama vipi tunavyo zieleza Aya ili wapate kufahamu.
(66) Na watu wako wameikanusha, nayo ni Haki. Sema: Mimi sikuwakilishwa juu yenu.
(67) Kila khabari ina kipindi chake. Nanyi mtakuja jua.
(68) Na unapo waona wanao ziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingilie mazungumzo mengine. Na kama Shet'ani akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhaalimu.