(53) Na hivi ndivyo tunavyo wajaribu wao kwa wao, ili waseme: Ni hao ndio Mwenyezi Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanao shukuru?
(54) Na wanapo kujia wanao ziamini Ishara zetu waambie: Assalamu alaikum! Amani iwe juu yenu! Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya kwamba atakaye fanya uovu miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwenye maghfira na Mwenye kurehemu.
(55) Na ndio hivi tunavyo zieleza Ishara ili ibainike njia ya wakosefu.
(56) Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnao waomba badala ya Mwenyezi Mungu. Sema: mimi sifuati matamanio yenu. Hivyo nitakuwa nimepotea, na sitakuwa miongoni mwa walio ongoka.
(57) Sema: Mimi nipo kwenye sharia iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu Mlezi, nanyi mnaikanusha. Mimi sinacho hicho mnacho kihimiza. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa kuhukumu kuliko wote.
(58) Sema: Lau kuwa ninacho hicho mnacho kihimiza, ingeli kwisha katwa shauri baina yangu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu anawashinda wote kuwajua madhaalimu.
(59) Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinacho bainisha.