(158) Wanangoja jengine ila wawafikie Malaika, au awafikie Mola wako Mlezi, au zifike baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi? Siku zitakapo fika baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi, kuamini hapo hakutomfaa mtu kitu, ikiwa hakuwa ameamini kabla yake, au amefanya kheri katika Imani yake. Sema: Ngojeni, nasi pia tunangoja.
(159) Hakika walio igawa Dini yao na wakawa makundi makundi, huna ukhusiano nao wowote. Bila ya shaka shauri yao iko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawaambia yale waliyo kuwa wakiyatenda.
(160) Afanyae wema atalipwa mfano wake mara kumi. na afanyae ubaya hatalipwa ila sawa nao tu. Na wao hawatadhulumiwa.
(161) Sema: Kwa hakika mimi Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka, Dini iliyo sawa kabisa, ambayo ndiyo mila ya Ibrahim aliye kuwa mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
(162) Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
(163) Hana mshirika wake. Na hayo ndiyo niliyo amrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu.
(164) Sema: Je nitafute Mola Mlezi asiye kuwa Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ndiye Mola Mlezi wa kila kitu? Na kila nafsi haichumii ila nafsi yake. Na habebi mwenye kubeba mzigo wa mwenziwe. Kisha marejeo yenu ni kwa Mola wenu Mlezi, naye atakuambieni mliyo kuwa mkikhitalifiana.
(165) Naye ndiye aliye kufanyeni makhalifa wa duniani, na amewanyanyua baadhi yenu juu ya wengine daraja kubwa kubwa, ili akujaribuni kwa hayo aliyo kupeni. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.