(74) Na pale Ibrahim alipo mwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika opotofu ulio wazi.
(75) Na kadhaalika tulimwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini.
(76) Na ulipo muingilia usiku akiona nyota, akasema: Huyu ni Mola Mlezi wangu. Ilipo tua akasema: Siwapendi wanao tua.
(77) Alipo uona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Ulipotua akasema: Kama Mola Mlezi wangu hakuniongoa, nitakuwa katika kaumu walio potea.
(78) Na alipo liona jua linachomoza akasema: Huyu ndiye Mola Mlezi wangu. Huyu mkubwa kuliko wote. Lilipo tua, alisema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayo fanyia ushirikina.
(79) Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu sawa sawa kwa aliye ziumba mbingu na ardhi, wala mimi si miongoni mwa washirikina.
(80) Na watu wake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji juu ya Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ameniongoa? Wala siogopi hao mnao washirikisha naye, ila Mola wangu Mlezi akipenda kitu. Mola wangu Mlezi amekusanya ilimu ya kila kitu. Basi je, hamkumbuki?
(81) Na vipi nivikhofu hivyo mnavyo vishirikisha, hali nyinyi hamkhofu kuwa nyinyi mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakukiteremshia uthibitisho. Basi kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, kama nyinyi mnajua?