(82) Wale ambao wameamini, na hawakuchanganya imani yao na dhulma - hao ndio watakao pata amani na wao ndio walio ongoka.
(83) Na hizo ndizo hoja zetu tulizo mpa Ibrahim kuhojiana na watu wake. Tunamnyanyua kwa vyeo tumtakaye. Hakika Mola Mlezi wako ni Mwenye hikima na Mwenye ujuzi.
(84) Na tukamtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaakub. Kila mmoja wao tulimwongoa. Na Nuhu tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake tulimwongoa Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tunavyo walipa wafanyao wema.
(85) Na Zakaria na Yahya na Isa na Ilyas. Wote walikuwa miongoni mwa watu wema.
(86) Na Ismail, na Al Yasaa, na Yunus, na Lut'. Na wote tuliwafadhilisha juu ya walimwengu wote.
(87) Na kutokana na baba zao, na vizazi vyao na ndugu zao. Na tukawateuwa na tukawaongoa kwenye Njia iliyo nyooka.
(88) Hiyo ni hidaya ya Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo humhidi amtakaye katika waja wake. Na lau wangeli mshirikisha yangeli waharibikia waliyo kuwa wakiyatenda.
(89) Hao ndio tulio wapa Vitabu na hukumu na Unabii. Ikiwa hawa watayakataa hayo, basi tumekwisha yawakilisha kwa watu wasio yakataa.
(90) Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewahidi. Basi fuata hidaya yao. Sema: Mimi sikuombeni ujira. Haya hayakuwa ila ni mawaidha kwa walimwengu wote.