(69) Wala wamchao Mungu hawana jukumu lolote kwao, lakini ni kukumbusha, asaa wapate kujiepusha.
(70) Waachilie mbali walio ifanya dini yao ni mchezo na pumbao, na uhai wa dunia ukawaghuri. Nawe kumbusha kwayo, isije nafsi ikaangamizwa kwa sababu ya iliyo yachuma, nayo haina mlinzi wala mwombezi ila Mwenyezi Mungu. Na ingatoa kila fidia haitokubaliwa. Hao ndio walio angamizwa kwa sababu ya yale waliyo yachuma. Wao watapata kinywaji cha maji ya moto kabisa, na adhabu chungu.
(71) Sema: Je, tumuombe asiye kuwa Mwenyezi Mungu ambae hatufai wala hatudhuru, na turejee nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuhidi? Tuwe kama ambao mashet'ani wamempumbaza katika ardhi, amebabaika? Anao marafiki wanao mwita ende kwenye uwongofu, wakimwambia: Njoo kwetu! Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio Uwongofu. Nasi tumeamrishwa tusilimu kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote,
(72) Na mshike Sala, na mcheni Yeye, na kwake Yeye ndiko mtako kusanywa.
(73) Naye ndiye aliye ziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Na anaposema: Kuwa! Basi huwa. Kauli yake ni Haki. Na ufalme wote ni wake Siku litapo pulizwa barugumu, Mjuzi wa yaliyo fichikana na yanayo onekana. Naye ndiye Mwenye hikima na Mwenye khabari.