(125) Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumhidi humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na anaye taka apotee hukifanya kifua chake kina dhiki, kimebana, kama kwamba anapanda mbinguni. Namna hivi Mwenyezi Mungu anajaalia uchafu juu ya wasio amini.
(126) Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi Iliyo nyooka. Tumezipambanua Aya kwa watu wanao kumbuka.
(127) Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao. Naye ndiye Rafiki Mlinzi wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyatenda.
(128) Na ile Siku atapo wakusanya wote awaambie: Enyi makundi ya majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanaadamu. Na marafiki zao katika wanaadamu waseme: Mola Mlezi wetu! Tulinufaishana sisi na wao. Na tumefikia ukomo wetu ulio tuwekea. Basi Mwenyezi Mungu atasema: Moto ndio makaazi yenu, mtadumu humo, ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye hikima, na Mwenye kujua.
(129) Ndio kama hivi tunawaelekeza madhaalimu wapendane wao kwa wao kwa sababu ya waliyo kuwa wakiyachuma.
(130) Enyi makundi ya majini na watu! Je, hawakukujieni Mitume kutokana na nyinyi wenyewe wakikubainishieni Aya zangu, na wakikuonyeni mkutano wa Siku yenu hii. Nao watasema: Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu. Na yaliwadanganya maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa makafiri.
(131) Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako Mlezi hakuwa wa kuiangamiza miji kwa dhulma, hali wenyewe wameghafilika.