(102) Na unapo kuwa pamoja nao, ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao. Na watakapo maliza sijida zao, basi nawende nyuma yenu, na lije kundi jingine ambalo halijasali, lisali pamoja nawe. Nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walio kufuru wanapenda mghafilike na silaha zenu na vifaa vyenu ili wakuvamieni mvamio wa mara moja. Wala si vibaya kwenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
(103) Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa kulala. Na mtapo tulia basi shikeni Sala kama dasturi. Kwani hakika Sala kwa Waumini ni faradhi iliyo wekewa nyakati maalumu.
(104) Wala msifanye ulegevu kuwafukuzia kaumu ya maadui. Ikiwa mnaumia, basi nao pia wanaumia kama mnavyo umia nyinyi. Nanyi mnataraji kwa Mwenyezi Mungu wasio yataraji wao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima.
(105) Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa haki ili upate kuhukumu baina ya watu kwa alivyo kuonyesha Mwenyezi Mungu. Wala usiwe mtetezi wa makhaaini.