(106) Na muombe maghfira Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
(107) Wala usiwatetee wanao khini nafsi zao. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi aliye khaaini, mwenye dhambi.
(108) Wanataka kujificha kwa watu, wala hawataki kujificha kwa Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja nao pale wanapo panga njama usiku kwa maneno asiyo yapenda. Na Mwenyezi Mungu anayajua vyema wanayo yatenda.
(109) Hivyo nyinyi mmewatetea hawa katika uhai huu wa duniani. Basi nani atakaye watetea kwa Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama? Au ni nani atakuwa wakili wao wa kumtegemea?
(110) Na anaye tenda uovu au akajidhulumu nafsi yake, kisha akaomba maghfira kwa Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
(111) Na anaye chuma dhambi, basi ameichumia nafsi yake mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hikima.
(112) Na atendaye kosa au dhambi kisha akamsingizia asiye na kosa, basi amejitwika dhulma na dhambi iliyo wazi.
(113) Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, kundi moja kati yao linge dhamiria kukupoteza. Wala hawapotezi ila nafsi zao, wala hawawezi kukudhuru kwa lolote. Na Mwenyezi Mungu amekuteremshia Kitabu na hikima na amekufundisha uliyo kuwa huyajui. Na fadhila za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako ni kubwa.