(141) Wale ambao wanakungojeeni, mkipata ushindi unao toka kwa Mwenyezi Mungu wao husema: Si tulikuwa pamoja nanyi vile? Na ikiwa ni sehemu ya makafiri kushinda wao huwaambia: Hatukuwa ni waweza wa kukushindeni, nasi tukakukingeni na hawa Waumini? Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama, wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini.
(142) Hakika wanaafiki wanamkhadaa Mwenyezi Mungu, na hali ni Yeye ndiye mwenye kuwakhadaa wao. Na wanapo inuka kusali huinuka kwa unyong'onyo, wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila kidogo tu.
(143) Wanayumba yumba baina ya huku na huko. Huku hawako na huko hawako. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, kabisa hutompatia njia.
(144) Enyi mlio amini! Msiwafanye makafiri kuwa ndio marafiki badala ya Waumini. Je, mnataka Mwenyezi Mungu awe na hoja iliyo wazi juu yenu?
(145) Hakika wanaafiki watakuwa katika t'abaka ya chini kabisa Motoni, wala hutompata yeyote wa kuwanusuru.
(146) Isipo kuwa wale walio tubu, na wakatengeneza na wakashikamana na Mwenyezi Mungu, na wakamtakasia Dini yao Mwenyezi Mungu. Basi hao ni pamoja na Waumini. Na Mwenyezi Mungu atakuja wapa Waumini ujira mkubwa.
(147) Mwenyezi Mungu hakuadhibuni mkimshukuru na mkamuamini. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kupokea shukrani na ndiye Mwenye kujua.