(163) Hakika Sisi tumekuletea wahyi wewe kama tulivyo wapelekea wahyi Nuhu na Manabii walio kuwa baada yake. Na tulimpelekea wahyi Ibrahim na Ismail na Is-haka na Yaakub na wajukuu zake, na Isa na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman, na Daud tukampa Zaburi.
(164) Na Mitume tulio kwisha kukuhadithia kabla yake, na Mitume wengine hatukukuhadithia. Na Mwenyezi Mungu alinena na Musa kwa maneno.
(165) Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(166) Lakini Mwenyezi Mungu anayashuhudia aliyo kuteremshia wewe. Ameyateremsha kwa kujua kwake - na Malaika pia wanashuhudia. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi.
(167) Hakika walio kufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, wamekwisha potelea mbali.
(168) Hakika wale walio kufuru na wakadhulumu hawi Mwenyezi Mungu kuwasamehe wala kuwaongoa njia.
(169) Isipo kuwa njia ya Jahannamu. Humo watadumu milele. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
(170) Enyi Watu! Amekwisha kujieni Mtume huyu na haki itokayo kwa Mola wenu Mlezi. Basi aminini, ndiyo kheri yenu. Na mkikakanusha basi hakika viliomo mbinguni na duniani ni vya Mwenyezi Mungu tu. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi Mwenye hikima.