(20) Na mkitaka kubadilisha mke mahali pa mke, na hali mmoja wao mmempa chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mtachukua kwa dhulma na kosa lilio wazi?
(21) Na mtachukuaje na ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi kwa nyinyi, na wao wanawake wamechukua kwenu ahadi iliyo madhubuti?
(22) Wala msiwaoe wake walio waoa baba zenu, ila yaliyo kwisha pita. Hakika huo ni uchafu na uchukizo na ni njia mbaya.
(23) Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa ndugu mume, na binti wa dada, na mama zenu walio kunyonyesheni, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu walio zaliwa na wake zenu mlio waingilia. Ikiwa hamkuwaingilia basi hapana lawama juu yenu. (Pia mmeharimishwa) wake wa watoto wenu walio toka katika migongo yenu. Na kuwaoa pamoja dada wawili isipo kuwa yale yaliyo kwisha pita. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.