(148) MWENYEZI MUNGU hapendi uovu uenezwe kwa maneno ila kwa mwenye kudhulumiwa. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.
(149) Mkidhihirisha wema au mkiuficha, au mkiyasamehe maovu, hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Muweza.
(150) Hakika wale wanao mkataa Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanataka kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, kwa kusema: Wengine tunawaamini na wengine tunawakataa. Na wanataka kushika njia iliyo kati kati ya haya,
(151) Hao ndio makafiri kweli. Na tumewaandalia makafiri adhabu ya kudhalilisha.
(152) Na walio muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala wasimfarikishe yeyote kati yao, hao atawapa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, na Mwenye kurehemu.
(153) Watu wa Kitabu wanakutaka uwateremshia kitabu kutoka mbinguni. Na kwa hakika walikwisha mtaka Musa makubwa kuliko hayo. Walisema: Tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi. Wakapigwa na radi kwa hiyo dhulma yao. Kisha wakamchukua ndama kumuabudu, baada ya kwisha wajia hoja zilizo wazi. Nasi tukasamehe hayo, na tukampa Musa nguvu zilizo dhaahiri.
(154) Na tukanyanyua mlima juu yao kwa kufanya agano nao. Na tukawaambia: Ingilieni mlangoni kwa unyenyekevu. Na tukawaambia: Msiivunje Siku ya Sabato (Jumaa mosi). Na tukachukua kwao ahadi iliyo madhubuti.