(87) Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Kwa yakini atakukusanyeni Siku ya Kiyama. Halina shaka hilo. Na ni nani msema kweli kuliko Mwenyezi Mungu?
(88) Mmekuwaje kuwa makundi mawili kwa khabari ya wanaafiki, na hali Mwenyezi Mungu amewageuza kwa sababu ya yale waliyo yachuma? Je! Mnataka kumwona mwongofu ambaye Mwenyezi Mungu amemhukumu kuwa kapotea? Na aliye mhukumu Mwenyezi Mungu kuwa amekwisha potea wewe hutampatia njia.
(89) Wanapenda lau kuwa nanyi mnge kufuru kama walivyo kufuru wao, ili muwe sawa sawa. Basi msiwafanye marafiki miongoni mwao mpaka wahame kwa ajili ya Dini ya Mwenyezi Mungu. Na wakikengeuka basi wakamateni na wauweni popote mnapo wapata. Wala msimfanye rafiki katika wao wala msaidizi.
(90) Isipokuwa wale walio fungamana na watu ambao mna ahadi baina yenu na wao, au wanakujieni na vifua vyao vina dhiki kupigana nanyi, au kupigana na watu wao. Na lau angeli penda Mwenyezi Mungu angeli wasaliti juu yenu wakapigana nanyi. Basi wakijitenga nanyi, wasipigane nanyi, na wakakuleteeni amani, basi Mwenyezi Mungu hakukupeni njia kupigana nao.
(91) Mtawakuta wengine wanataka wapate salama kwenu na salama kwa watu wao. Kila wakirudishwa kwenye fitna hudidimizwa humo. Ikiwa hawajitengi nanyi, na wakakuleteeni salama, na wakazuia mikono yao, basi wakamateni na wauweni popote mnapo wakuta. Na juu ya hao ndio tumekupeni hoja zilizo wazi.