(122) Na wale walio amini na wakatenda mema, tutawaingiza katika Bustani zipitayo mito kati yake. Watadumu humo milele. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo kweli. Na nani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Mwenyezi Mungu.
(123) Si kwa matamanio yenu, wala matamanio ya Watu wa Kitabu! Anaye fanya ubaya atalipwa kwalo, wala hatajipatia mlinzi wala wa kumnusuru, isipo kuwa Mwenyezi Mungu.
(124) Na anaye fanya mema, akiwa mwanamume au mwanamke, naye ni Muumini - basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa hata kadiri ya tundu ya kokwa ya tende.
(125) Na nani aliye bora kwa dini kuliko yule aliye usilimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye akawa mwema, na anafuata mila ya Ibrahim mwongofu? Na Mwenyezi Mungu alimfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwendani.
(126) Ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo duniani. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuvizunguka vitu vyote.
(127) Wanakuuliza nini sharia ya wanawake. Sema: Mwenyezi Mungu ana kutoleeni fatwa juu yao, na mnayo somewa humu Kitabuni kukhusu mayatima wanawake ambao hamwapi walicho andikiwa, na mnapenda kuwaoa, na kukhusu wanyonge katika watoto, na kwamba mwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na kheri yoyote mnayo fanya Mwenyezi Mungu anaijua.