(155) Basi kwa sababu ya kuvunja kwao ahadi zao, na kuzikataa kwao ishara za Mwenyezi Mungu, na kuwauwa kwao Manabii bila ya haki, na kusema kwao: Nyoyo zetu zimefumbwa; bali Mwenyezi Mungu amezipiga muhuri kwa kufuru zao, basi hawaamini ila kidogo tu -
(156) Na pia kwa kufuru zao na kumsingizia kwao Maryamu uwongo mkubwa,
(157) Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masihi Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu - nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini.
(158) Bali Mwenyezi Mungu alim- tukuza kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
(159) Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao.
(160) Basi kwa dhulma yao Mayahudi tuliwaharimishia vitu vizuri walivyo halalishiwa. Na kwa sababu ya kuwazuilia kwao watu wengi na Njia ya Mwenyezi Mungu,
(161) Na kuchukua kwao riba, nao wamekatazwa, na kula kwao mali ya watu kwa dhulma. Basi tumewaandalia makafiri katika wao adhabu yenye uchungu.
(162) Lakini walio bobea katika ilimu miongoni mwao, na Waumini, wanayaamini uliyo teremshiwa wewe, na yaliyo teremshwa kabla yako. Na wanao shika Sala, na wakatoa Zaka, na wanao muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho - hao tutawapa malipo makubwa.