(60) Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo teremshwa kwako na yaliyo teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Na Shet'ani anataka kuwapotezelea mbali.
(61) Na wanapo ambiwa: Njooni kwenye yale aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, na njooni kwa Mtume; utawaona wanaafiki wanakukwepa kwa upinzani.
(62) Basi inakuwaje unapo wasibu msiba kwa sababu ya yale iliyo tanguliza mikono yao? Hapo tena hukujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu wakisema: Hatukutaka ila wema na mapatano.
(63) Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo ndani ya nyoyo zao. Basi waachilie mbali, uwape mawaidha na uwaambie maneno ya kuathiri na kuingia katika nafsi zao.
(64) Na hatukumtuma Mtume yeyote ila at'iiwe kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na lau pale walipo jidhulumu nafsi zao wangeli kujia, wakamwomba Mwenyezi Mungu msamaha, na Mtume akawaombea msamaha, hapana shaka wangeli mkuta Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
(65) La! Naapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye muamuzi katika yale wanayo khitalifiana, kisha wasione uzito katika nyoyo zao juu ya hukumu utayo toa, na wanyenykee kabisa.