(27) Na Mwenyezi Mungu anataka kukurejezeni kwenye ut'iifu wake, na wanao taka kufuata matamanio wanataka mkengeuke makengeuko makubwa.
(28) Mwenyezi Mungu anataka kukupunguzieni taabu, na mwanaadamu ameumbwa dhaifu.
(29) Enyi mlio amini! Msiliane mali yenu kwa dhulma, isipo kuwa iwe biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni.
(30) Na mwenye kutenda hayo kwa uadui na udhaalimu, basi huyo tutamwingiza Motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu.
(31) Mkiyaepuka makubwa mnayo katazwa, tutakufutieni makosa yenu madogo, na tutakuingizeni mahali patukufu.
(32) Wala msitamani alicho wafadhili Mwenyezi Mungu baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wana fungu katika walio vichuma, na wanawake wana fungu katika walio vichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
(33) Na kila mmoja tumemwekea warithi katika waliyo yaacha wazazi wawili na jamaa. Na mlio fungamana nao ahadi wapeni fungu lao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.