(113) Na Mayahudi husema: Wakristo hawana lao jambo. Na Wakristo husema: Mayahudi hawana lao jambo. Na ilhali wote wanasoma Kitabu hicho hicho (Biblia). Na kadhaalika walisema wale wasio jua kitu mfano wa kauli yao hii. Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyo kuwa wakikhitilafiana.
(114) Na ni nani dhaalimu mkubwa kuliko yule anaye zuia misikiti ya Mwenyezi Mungu kutajwa ndani yake jina lake na akajitahidi kuiharibu? Watu hao haitawafalia kuingia humo ila nao wanaogopa. Duniani watapata hizaya na Akhera watapata adhabu kubwa.
(115) Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnako elekea, huko Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye wasaa na Mjuzi.
(116) Na ati wanasema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu! Ametakasika na hayo. Bali vyote viliomo mbinguni na duniani ni vyake. Vyote vinamt'ii Yeye.
(117) Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina ruwaza; na anapo taka jambo basi huliambia tu: Kuwa! Nalo huwa.
(118) Na walisema wale wasio jua kitu: Mbona Mwenyezi Mungu hasemi nasi au zikatufikia Ishara. Kama hivyo walisema wale walio kuwa kabla yao mfano wa kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi tumeziweka wazi Ishara kwa watu wenye yakini.
(119) Hakika Sisi tumekutuma kwa Haki uwe mbashiri, na mwonyaji. Na wala hutaulizwa juu ya watu wa Motoni.