(154) Wala msiseme kuwa wale walio uwawa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti; bali hao ni wahai, lakini nyinyi hamtambui.
(155) Hapana shaka tutakujaribuni kwa chembe ya khofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na matunda. Na wabashirie wanao subiri,
(156) Wale ambao ukiwasibu msiba husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea.
(157) Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Nao ndio wenye kuongoka.
(158) Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi anaye hiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anaye jitendea mwenyewe kheri basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na Mjuzi.
(159) Hakika wale wanao ficha tuliyo yateremsha -- nazo ni hoja zilizo wazi na uwongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni -- hao anawalaani Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani.
(160) Ila wale walio tubu na wakatengeneza na wakabainisha, basi hao nitapokea toba yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
(161) Hakika walio kufuru na wakafa hali ni makafiri, hao iko juu yao laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.
(162) Watadumu humo. Hawata-punguziwa adhabu wala hawatapewa muda wa kupumzika.
(163) Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.