(62) Hakika Walio amini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akatenda mema basi watapata malipwa yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.
(63) Na tulipo chukua ahadi yenu, na tukaunyanyua mlima juu yenu (tukakwambieni): Shikeni kwa nguvu haya tuliyo kupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kujilinda.
(64) Kisha mligeuka baada ya haya. Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema zake, mngeli kuwa miongoni mwa wenye kukhasirika.
(65) Na hakika mlikwisha yajua ya wale miongoni mwenu walio ivunja Sabato, (siku ya mapumziko, Jumaa Mosi) na tukawaambia: Kuweni manyani wadhalilifu.
(66) Kwa hivyo tukayafanya hayo kuwa onyo kwa wale walio kuwa katika zama zao na walio kuja baada yao, na mawaidha kwa wachamngu.
(67) Na Musa alipo waambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje ng'ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: Audhubil lahi! Najikinga kwa Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga.
(68) Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni ng'ombe gani? Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba ng'ombe huyo si mpevu, wala si kinda, bali ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyo amrishwa.
(69) Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie nini rangi yake? Akasema: Yeye anasema, kuwa ng'ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imekoza, huwapendeza wanao mtazama.