(249) Basi Taluti alipo ondoka na majeshi alisema: Mwenyezi Mungu atakujaribuni kwa mto. Atakaye kunywa humo si pamoja nami, na asiye kunywa atakuwa pamoja nami: ila atakaye teka kiasi ya kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipo kuwa wachache tu miongoni mwao. Alipo vuka mto yeye na wale walio amini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
(250) Na walipo toka kupambana na Jaluti na majeshi yake walisema: Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na utusaidie tuwashinde watu Makafiri--
(251) --Kwa idhini ya Mwenyezi Mungu waliwatimua, na Daudi akamuuwa Jaluti, na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hikima, na akamfundisha aliyo yapenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawapambanishi watu kwa watu basi dunia ingeli haribika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya walimwengu wote.
(252) Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.