(270) Na chochote mnacho toa au nadhiri mnazo weka basi hakika Mwenyezi Mungu anajua. Na walio dhulumu hawana wa kuwanusuru.
(271) Mkizidhihirisha sadaka ni vizuri; na mkizificha mkawapa mafakiri kwa siri basi hivyo ni kheri kwenu, na yatakuondoleeni baadhi ya maovu yenu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayo yatenda.
(272) Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na kheri yoyote mnayo toa ni kwa nafsi zenu. Wala msitoe ila kwa kutafuta wajihi wa Mwenyezi Mungu. Na kheri yoyote mtakayo toa mtalipwa kwa ukamilifu, wala hamtadhulumiwa.
(273) Nawapewe mafakiri walio zuilika katika njia za Mwenyezi Mungu, wasio weza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiye wajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama zao; hawang'ang'analii watu kwa kuwaomba. Na kheri yoyote mnayo toa, basi kwa yakini Mwenyezi Mungu anaijua.
(274) Wale wanao toa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhaahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika.