(58) Na tulipo sema: Ingieni mji huu, na humo mle mpendapo maridhawa, na ingieni katika mlango wake kwa unyenyekevu, na semeni: Tusamehe! Tutakusameheni makosa yenu, na tutawazidishia wema wafanyao wema.
(59) Lakini walio dhulumu waliibadili kauli isiyo kuwa waliyo ambiwa. Kwa hivyo tukaiteremsha juu ya wale walio dhulumu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya walivyo kuwa wamepotoka.
(60) Na Musa alipo omba maji kwa ajili ya watu wake, tulimwambia: Lipige jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatimbuka chemchem kumi na mbili; kila kabila ikajua mahali pake pa kunywea. Tukawaambia: Kuleni na mnywe riziki ya Mwenyezi Mungu, wala msiasi katika nchi mkafanya uharibifu.
(61) Na mlipo sema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu, basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyo mea katika ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na thom zake, na adesi zake, na vitunguu vyake. Akasema: Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyo viomba. Na wakapigwa na unyonge, na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyo asi na wakapindukia mipaka.