(177) Sio wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anaye muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii, na anawapa mali, kwa kupenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ugombozi, na akawa anashika Sala, na akatoa Zaka, na wanao timiza ahadi yao wanapo ahidi, na wanao vumilia katika shida na dhara na wakati wa vita; hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wajilindao.
(178) Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika walio uwawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kuliko tokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakaye vuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu.
(179) Mtakuwa nao uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi wenye akili, ili msalimike.
(180) Mmeandikiwa -- mmoja wenu anapo fikwa na mauti, kama akiacha mali -- afanye wasia kwa wazazi wake na jamaa zake kwa namna nzuri inayo pendeza. Ni waajibu haya kwa wachamngu.
(181) Na atakaye ubadilisha wasia baada ya kuusikia, basi dhambi yake ni juu ya wale watakao ubadilisha; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.