(253) MITUME hao tumewatukuza baadhi yao juu ya wengineo. Katika wao wapo ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na wengine akawapandisha vyeo. Na tukampa Isa mwana wa Mariyam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana walio kuwa baada yao baada ya kuwajia hoja zilizo wazi. Lakini walikhitalifiana. Basi wapo kati yao walio amini, na wengine kati yao walio kufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu alipenda wasingeli pigana. Lakini Mwenyezi Mungu hutenda atakavyo.
(254) Enyi mlio amini! Toeni katika tulivyo kupeni kabla haijafika Siku ambayo hapatakuwapo biashara, wala urafiki, wala uombezi. Na makafiri ndio madhaalimu.
(255) Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu.
(256) Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu. Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.