(182) Na mwenye kumkhofia muusiaji kwenda kombo au kupata dhambi akasuluhisha baina yao, basi hatakuwa na dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.
(183) Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.
(184) (Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.
(185) Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.
(186) Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.